Moduli 10 kati ya 10

Ni Mustakabali Gani Bitcoin Inaweza Kujenga?

10.0 Utangulizi

Bitcoin ni zaidi ya sarafu; ni mapinduzi yanayorejesha mamlaka kwa watu, yakitoa ladha ya amani na uhuru katika dunia inayotamani kupewa nguvu.My First Bitcoin

Katika moduli hii ya mwisho, tutahitimisha masomo tuliyojifunza katika safari yetu, tutauliza na kujadili maswali muhimu kadhaa, na kuchunguza mustakabali wa Bitcoin.

Bitcoin si teknolojia tu; ni mtandao unaowezesha aina mpya ya pesa ambayo ugavi wake hauwezi kubadilishwa na mtu mmoja. Binadamu hawajawahi kuwa na aina ya pesa yenye ugavi usiobadilika na isiyodhibitiwa na mamlaka kuu. Ikiwa itakubaliwa na wengi, Bitcoin ni chombo kitakachofungua harakati za mabadiliko chanya ambazo zinaweza kubadilisha maisha ya watu duniani kote. Inawakilisha mapinduzi ya amani kuelekea uhuru wa pamoja na usawa, ikifungua fursa mpya kwa binadamu kwa kuunda mfumo wa pesa wa pamoja na wa kimataifa.

Kama mfumo wa kimataifa usio na udhibiti wa kati, Bitcoin inawawezesha watu kuwa na uhuru zaidi wa kifedha, ikihamisha mamlaka kutoka kwa wachache kwenda kwa wengi. Inatoa jukwaa salama, lisiloweza kudhibitiwa kwa urahisi, la kuhifadhi na kuhamisha thamani, na kuwawezesha watu binafsi kuchukua udhibiti wa mali zao na kulinda uwezo wao wa kununua. Hili ni muhimu sana katika mazingira ya sasa ya uchumi usiotabirika, ambapo mfumo wa kifedha wa jadi unakabiliwa na changamoto ambazo hazijawahi kutokea.

Ifuatayo, tutaangalia aina nyingine ya sarafu ya kidijitali inayoitwa Sarafu ya Kidijitali ya Benki Kuu (CBDC) na kutathmini jinsi inavyofanana na kutofautiana na Bitcoin.

10.1 Sarafu za Kidijitali za Benki Kuu (CBDCs) ni aina ya sarafu ya kidijitali inayotolewa na kusimamiwa na benki kuu ya nchi. Tofauti na fedha za kawaida za karatasi au sarafu, CBDCs zipo katika mfumo wa kidijitali pekee na zinawakilisha dhamana rasmi ya serikali. Lengo la CBDCs ni kutoa njia salama na rahisi ya kufanya miamala, kuongeza ufanisi wa mfumo wa malipo, na kutoa udhibiti zaidi kwa benki kuu juu ya sera za fedha. Tofauti na Bitcoin au sarafu nyingine za kidijitali zisizo na mamlaka kuu, CBDCs zinadhibitiwa kikamilifu na benki kuu na serikali.

Fedha za Kidijitali za Benki Kuu, au CBDCs, ni matoleo ya kidijitali ya pesa za kawaida za fiat. CBDCs zinafuata sheria zilezile kama pesa za fiat, ambapo mamlaka kuu (kama serikali) inaweza kuongeza usambazaji wa pesa bila ridhaa ya mtu yeyote, na hivyo kupunguza uwezo wa watu kununua vitu. Hata hivyo, CBDCs pia zinawapa serikali zana mpya na zenye nguvu za kudhibiti jinsi pesa hizo zinavyotumiwa na watu duniani kote.

Kulingana na utafiti wa Human Rights Foundation (HRF), nchi 134 na vyama vya sarafu, vinavyowakilisha 98% ya Pato la Taifa Duniani, vinachunguza CBDC. Mnamo Mei 2020 idadi hiyo ilikuwa ni 35 tu. Kwa sasa, nchi 66 ziko katika hatua za juu za uchunguzi—maendeleo, majaribio, au uzinduzi. Kila nchi ya G20 inachunguza CBDC, na 19 kati yao ziko katika hatua za juu za uchunguzi wa CBDC.

Unaweza kuangalia kama nchi yako inajaribu CBDCs kwenye tovuti ya Human Rights Foundation ya kufuatilia CBDC kupitia cbdctracker.hrf.org au cbdctracker.org

Kwa hiyo, mbali na kuwa za kidijitali, ni nini kinachofanya CBDCs kuwa tofauti na pesa za kawaida za fiat? Ni muhimu kuelewa kwamba, tofauti na pesa za kawaida za fiat katika mfumo wa noti au sarafu, CBDCs zinairuhusu serikali kufuatilia na kudhibiti kila muamala wa kidijitali duniani kote. Hii inamaanisha serikali inaweza kusitisha miamala fulani au hata kugandisha akaunti yako yote ikiwa hawakupendi au hawapendi jinsi unavyotumia pesa zako.

Kwa mfano, fikiria unataka kutuma pesa kwa mwanafamilia katika nchi inayohitaji msaada, lakini serikali yako ya ndani inakataa muamala wako kwa sababu hawakubaliani na viongozi wa nchi hiyo. Au fikiria unaenda dukani kununua kitu unachokipenda, lakini huwezi kwa sababu ulitoa maoni yako kwa uhuru kwenye mitandao ya kijamii.

Kwa sasa, pesa nyingi za fiat zinazozunguka tayari ni za kidijitali — tofauti ikiwa ni kwamba ni benki mbalimbali zinazoweza kufuatilia na kuzuia miamala, na ni ile tu inayopita kwenye akaunti zao. Hata hivyo, mifano ya udhibiti kama ilivyo hapo juu imetokea na inaendelea kutokea katika nchi nyingi, ikitekelezwa na benki lakini mara nyingi kwa maagizo ya serikali kuu.

CBDCs, hata hivyo, zinawapa serikali udhibiti mkubwa juu ya jinsi pesa zinavyotumiwa katika mamlaka yao, na hivyo kupunguza uwezo wa watu kutumia pesa zao kwa uhuru. Baadhi ya watu wanasema kwamba CBDCs zinaweza kuruhusu serikali kutekeleza sera mara moja, bila uingiliaji wa binadamu. Badala ya kushirikiana na benki nyingi, wanaweza kufuatilia na kuzuia mtiririko wa pesa haraka ndani ya nchi yao.

CBDC Bitcoin
Ugavi usio na kikomo Ugavi wenye kikomo
Imejikita sehemu moja Imejikita sehemu nyingi
Sera ya fedha isiyo wazi Sera ya fedha iliyo wazi
Imefungwa & inahitaji ruhusa Wazi & haihitaji ruhusa
Hatari ya kutaifishwa Haiwezi kutwaliwa
Inavunja faragha Inalinda faragha
Inaruhusu udhibiti Inapingana na udhibiti

CBDCs na Bitcoin zote ni za kidijitali lakini, zaidi ya kufanana huku, zinawakilisha aina tofauti kabisa za pesa zenye falsafa tofauti, na hivyo kusababisha matokeo tofauti.

10.2 Falsafa ya Bitcoin

Katika Moduli ya 5 na 8, tuligundua kwamba watu wanaoendesha nodi husaidia kulinda sheria za Bitcoin. Hili ni jambo kubwa kwa sababu, kwa mara ya kwanza kabisa, watu kama sisi tunaweza kuwa sehemu ya mtandao unaohakikisha sheria za mfumo wetu wa fedha zinalindwa. Sheria hizi zinajumuisha upatikanaji mdogo wa pesa, na hakuna mtu mmoja anayeweza kubadilisha sheria hizi. Hii ni fursa ya kipekee kwa watu wa kawaida kushiriki katika kulinda pesa zetu ziwe salama na za kuaminika.

Falsafa ya Bitcoin ni ya kuwezesha watu, uhuru, kujitegemea kifedha, kufikiri kwa kina, na kujichagulia — wazo kwamba sote tunapaswa kuwa na sauti katika sheria za mfumo tunaouchagua sisi wenyewe. Tofauti na mfumo wa fiat unaodhibitiwa na mamlaka kuu zenye nguvu, Bitcoin inategemea mtandao ambapo hakuna mtu mmoja mwenye udhibiti wote. Hii inamaanisha hakuna mtu anayeweza kuchukua mali yako au kukuzuia kutumia pesa zako unavyotaka. Kinyume chake ndicho kinachotokea kwa CBDC.

Katika dunia ya fiat, kuwa na utajiri zaidi kunamaanisha kuwa na ushawishi na udhibiti zaidi. Kinyume chake, Bitcoin inagawa mamlaka kwa watu wote kwa usawa. Ni juhudi ya pamoja ambapo kila mtu, bila kujali ana pesa kiasi gani, anacheza jukumu muhimu katika mfumo. Fikiria kama nguvu ya pamoja, ambapo nguvu yako ya kifedha haiamui moja kwa moja ushawishi wako. Bitcoin imejengwa juu ya sheria zisizobadilika na, katika umoja huu, ni kama ubinadamu wenyewe unadhibiti mfumo. Sio watu wachache wenye nguvu wanaoamua — bali ni sisi sote tukifanya kazi pamoja kama jamii imara, tukiongoza mwelekeo wa Bitcoin bila mamlaka moja kubadilisha njia yake.

Wakati katika mfumo wa fiat wenye nguvu ndio wanaoweka sheria, katika mfumo wa Bitcoin ni mchango wa ziada wa watu binafsi unaoupa mtandao nguvu. Hakuna taasisi moja, bila kujali utajiri au mamlaka, inayoweza kuelekeza mwelekeo wa mfumo wa Bitcoin. Hii ni kubadilisha kabisa nguvu za jadi, ambapo uimara wa mfumo hauko mikononi mwa wachache bali ni nguvu ya pamoja ya washiriki wote.

Wazo kuu ni kuunda mfumo salama, wazi, na wa haki ambapo kila mtu anaweza kupata, kumiliki, na kutumia pesa za dunia, bila kujali yeye ni nani au yuko wapi.

Tafakari: Je, Una Haki ya Kudhibiti Pesa Zako Mwenyewe?

  1. Je, upatikanaji wa pesa ni hitaji la kibinadamu na haki ya binadamu? Kwa nini?
  2. Ikiwa huwezi kutumia pesa zako unavyotaka, kuzituma kwa yeyote unayemtaka, au kuzichukua nawe kwenda nchi mpya, je, kweli ni zako? Kwa nini?
  3. Kwa nini biashara ya kubadilishana bidhaa iliacha kutumika? Tatizo la 'double coincidence of wants' ni nini?
  4. Kwa nini ni muhimu kuelewa tukio la Nixon shock na umuhimu wake hadi leo?
  5. Ni tukio gani jingine la kihistoria tulilojifunza ambalo limekugusa zaidi?
  6. Pesa zenye upatikanaji wa kudumu zinatofautianaje na sarafu za fiat za kawaida?
  7. Bitcoin iliundwa lini, na nani, na kwa kusudi gani? Wazo la mfumo usio na mamlaka kuu linachangiaje katika dhamira hii?
  8. Ni faida na hasara zipi zinazohusiana na pochi za custodial na non-custodial? Ni pochi ipi uliyoipenda zaidi?
  9. Unajua nini kuhusu Lightning Network? Ungetumia kwa miamala gani?
  10. Kwa njia gani kuendesha nodi yako mwenyewe kunasaidia mtandao?
  11. Kudhibiti pesa zako mwenyewe kunawezaje kukuimarisha katika maisha ya kila siku na mipango yako ya baadaye?
  12. Ni kwa njia zipi uhuru wa kifedha unaweza kuongeza uwezo wako wa kuchangia vyema katika jamii yako au kwa jamii kwa ujumla?

10.3 Faida za Bitcoin

Hyperbitcoinization inahusu mustakabali wa kubuniwa ambapo Bitcoin imekuwa mfumo mkuu wa fedha duniani. Hii ingemaanisha kwamba Bitcoin inatumika na kila mtu, kila mahali, na kwa kila kitu — kuanzia kununua kahawa hadi kulipa bili, na hata kununua mali. Kuongezeka kwa hamasa kuhusu Bitcoin miongoni mwa watu binafsi, biashara, na hata serikali kunaonyesha athari inayoweza kutokea kutokana na kupokelewa kwake kote duniani kwenye uchumi na jamii kwa ujumla.

Haya ni baadhi ya manufaa ya dunia iliyo na hyperbitcoinization:

Mustakabali wa Kujitawala Kibinafsi

Mustakabali wa kujitawala kibinafsi ni ule ambapo watu duniani kote wanakuwa na udhibiti kamili juu ya utambulisho wao wa kidijitali na mali zao. Hii inaweza kusababisha ushirikishwaji mkubwa wa kifedha, uhuru, faragha, na usalama, hivyo kuchangia ustawi mkubwa wa binadamu, wingi, na furaha kwa ujumla.

Hifadhi ya Thamani Inayoaminika

Upungufu wa kidijitali wa Bitcoin unaifanya kuwa hifadhi ya thamani inayoaminika zaidi kwa muda mrefu, jambo ambalo linawahamasisha watu wengi zaidi kuitumia kama njia ya kuweka akiba kwa ajili ya siku zijazo.

Mabadiliko katika Sera ya Fedha

Ikiwa Bitcoin itapokelewa kwa wingi, inaweza kuondoa uwezo wa serikali kuongeza mzunguko wa fedha kupitia zana za jadi za sera ya fedha. Kupokelewa kwa Bitcoin kwa wingi kunaweza kuongeza uwezo wa ununuzi wa watu na kuhamasisha jamii kuelekea mtazamo wa kipaumbele cha muda mrefu.

Uwazi na Ufuatiliaji Ulioimarishwa

Rekodi isiyoweza kubadilishwa na isiyoweza kuchezewa ya miamala yote kwenye blockchain ingeongeza uwazi na uwajibikaji katika sekta na viwanda mbalimbali. Kwa sasa, taasisi zenye nguvu zina uwezo wa kuhamisha mabilioni ya shilingi duniani bila uwazi wa kutosha kuhusu fedha hizo zinakoenda au jinsi zinavyotumika. Kwa kutoa rekodi wazi na inayoweza kuthibitishwa ya miamala ya kifedha, Bitcoin inaweza kuhakikisha kwamba uhamishaji wa mitaji unakuwa wazi zaidi kwa umma.

Mapinduzi katika Soko la Uhawilishaji Fedha

Soko la uhawilishaji fedha linahusisha uhamishaji wa fedha kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine, mara nyingi kuvuka mipaka ya kimataifa. Licha ya kupungua kwa gharama, uhawilishaji fedha bado ni ghali ukilinganisha na uhamisho wa benki wa ndani, hasa kwa kiasi kidogo. Mtandao wa Lightning unatoa miamala ya haraka karibu papo hapo na kwa gharama nafuu duniani kote, na kuufanya ufae sana kwa soko la uhawilishaji fedha na kutatua changamoto za gharama kubwa na nyinginezo kama vile ucheleweshaji wa malipo na vikwazo vya saa za biashara.

Nishati ya Kutosha

Wakati kuna nishati ya kutosha na nafuu, jamii hunufaika, na sekta nyingi pamoja na jamii zinaweza kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya umeme majumbani, kwenye biashara, na kwenye teknolojia mpya. Uchimbaji wa Bitcoin unawapa wachimbaji motisha kutumia nishati ya ziada ambayo kawaida ingepotea kutoka kwenye vyanzo endelevu kama vile jua, upepo, na umeme wa maji. Wachimbaji wa Bitcoin wanaweza kutumia nishati hii ya ziada na nafuu kuzalisha bitcoin mpya kupitia shughuli za uchimbaji, kulinda mtandao, na kutoa nishati ya ziada waliyozalisha kurudi kwenye gridi ya nishati ya jamii inapohitajika.

10.4 Mustakabali Ulio na Uwezo

Pesa husaidia watu kuwasiliana ni shughuli, bidhaa, na huduma zipi zilizo muhimu zaidi katika jamii. Wakati pesa zinadhibitiwa na mamlaka za kati, bila shaka zitachezewa.

Moja ya makosa ambayo binadamu wamekuwa wakirudia katika historia ni kuingilia soko huru, kama vile kupitia udanganyifu wa pesa, jambo ambalo linaathiri vibaya watu binafsi, familia, biashara, na hatimaye ustawi wa binadamu duniani.

Kwa kuchukua udhibiti wa pesa mikononi mwa vyama vya kati na badala yake kutumia pesa zenye idadi isiyobadilika ambayo hakuna mtu mmoja anayeweza kubadilisha, tunaweza kuunda dunia tofauti kabisa — dunia ambayo hatuhitaji kuwaamini wanasiasa kufanya jambo sahihi, kwa sababu kufanya jambo lisilo sahihi kunakuwa ghali sana.

Hii ni dunia mpya kabisa. Na unaweza kuwa sehemu ya kuunda uhalisia huu. Kwa kutumia Bitcoin, kuendesha node yako mwenyewe, na kuwasaidia binadamu wenzako kujifunza zaidi kuhusu mustakabali wa pesa, unapiga kura kwa ajili ya dunia tofauti.

Shughuli: Majadiliano ya Mwisho — Mtazamo Wako Ulibadilika Vipi?

Tafadhali jibu maswali yafuatayo:

Kwa nini tunahitaji pesa?
Pesa ni nini?
Nani anadhibiti pesa?
Nini kinachofanya pesa ziwe na “thamani”?
Andika maswali yaliyoteuliwa wakati wa Moduli ya 1 na yajibu sasa
  1. Rudi kwenye shughuli ya kwanza katika Moduli ya 1 na linganisha majibu yako mapya na yale ya awali.
  2. Linganisha na jadili majibu na maswali ya awali. Je, kuna kitu kimebadilika?
  3. Jiulize swali hili la mwisho: Hatua yangu inayofuata ni ipi? Na ninawezaje kutumia maarifa haya mapya kujipa nguvu?

Kama uko tayari kuchukua hatua inayofuata, angalia rasilimali za ziada katika sehemu inayofuata, ambazo zina rasilimali bora zaidi za kujifunza zaidi na kufanikiwa.

Rasilimali
Bitcoin is Generational Wealth - A Short Film
Uwezekano wa mabadiliko chanya ni mkubwa, ndiyo maana tunakukaribisha utazame video hii ili kujifunza zaidi.

↑ Rudi kwenye jedwali la yaliyomo